Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la masuala ya Kiuchumi na Kijamii, ECOSOC, Collen Vixen Kelapile ameiteua nchi ya Tanzania kuwa Mwenyekiti Mwenza wa Jukwaa la Saba la Wadau Mbalimbali wa masuala ya Sayansi, Teknolojia na Uvumbuzi katika kutekeleza Agenda 2030 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, SDGs. 

 

Wakati huo huo Rais huyo wa ECOSOC amemteua Balozi Profesa Kennedy Gastorn ambaye ni Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, na Balozi Sergiy Kyslytsya, Mwakilishi wa Kudumu wa Ukraine katika Umoja wa Mataifa kuwa wenyeviti wa Jukwaa hilo. 

Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa tumepata fursa ya kuzungumza na Balozi Profesa Kennedy Gastorn na kwanza tukitaka kufahamu uteuzi huu una maana gani kwa Tanzania? 

“Ni heshima kubwa sana kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuweza kupata nafasi hii kuwa Mwenyekiti Mwenza wa Jukwaa hili,” Anaeleza Balozi Profesa Kennedy Gaston na kufafanua zaidi akisema, “pamoja na mambo mengine hii ishara ya jinsi ambavyo Tanzania na diplomasia yake inazidi kukubalika katika macho ya kimataifa  chini ya uongozi wa mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na Tanzania kama mwanachama mwingine katika Umoja wa Mataifa, itaitumia nafasi hii kuweza kubadilishana uzoefu na na kuonesha mipango yake, mafanikio na changamoto katika sekta hii na kuweza kukuza mahusiano na kubadilishana uzoefu na wadau wengine kimataifa. Lakini pia kama Mwenyekiti mweza Tanzania itatumia nafasi hii kuwaunganisha wadau wa masuala ya sayansi teknolojia na uvumbuzi katika kutekeleza ajenda ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030 ya Umoja wa Mataifa.” 

Je, jukwaa hili la wadau wa masuala ya Sayansi, Teknolojia na Uvumbuzi madhumuni yake ni nini? Balozi Kennedy anafafanua akisema, “madhumuni ya jukwaa hili ni kuwakutanisha wadau mbalimbali wa masuala ya sayansi, teknolojia na uvumbuzi ili kujadili na kubadilishana uzoefu kwa namna masuala hayo yanavyoweza kurahisisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, SDGs ya mwaka 2030.” 

Na kuhusu nini kitarajiwe na nchi wanachama mathalani nchi za Afrika Mashariki na Kati kutoka katika uongozi huu mpya wa Jukwaa? Balozi Kennedy Gastorn anasema, “matarajio makubwa ni mwendelezo wa ushirikiano wa kimataifa kati ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa pamoja na wadau mbalimbali katika sekta hii ya sayansi, teknolojia na uvumbuzi. Na matokeo ya majadiliano ya jukwaa hili yatawasilishwa kwenye mkutano wa wakuu wa nchi utakaofanyika mwezi Julai mwaka huu.”