Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutierres kwenye Makuu ya umoja huo na kujadiliana masuala kadhaa yakiwemo ya maendeleo ya jamii, ulinzi na usalama, siasa na ushirikiano wa Tanzania na UN.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano wao leo (Jumamosi, Septemba 21, 2024), Waziri Mkuu ambaye yuko Marekani akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA79), amesema katika suala la maendeleo ya jamii wamejadiliana umuhimu wa kuinua uwezo wa wananchi kiuchumi ikiwemo upatikanaji wa huduma zote muhimu.
Kuhusu ulinzi na usalama, Waziri Mkuu amesema Tanzania imepongezwa kwa kusimamia ukombozi wa nchi nyingi za Afrika hasa za SADC. “Sasa hivi Serikali yetu inaendelea kuunga mkono kwa kupeleka vikosi vya ulinzi kwenye nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na za SADC,” amesema.
“Katika hili, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amempongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wananchi na Serikali kwa ujumla katika kuhakikisha bara la Afrika linabaki kuwa salama.”
Kuhusu siasa, Waziri Mkuu amemweleza Katibu Mkuu huyo juu ya uwepo wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba, mwaka huu na uchaguzi mkuu ujao na kusisitiza haja ya mtu kushiriki uchaguzi huo na haki ya kuchaguliwa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu ameipongeza Tanzania kwa jinsi ilivyoshiriki kuisaidia Burundi kuwa salama kwa kuendelea kuwapokea wakimbizi katika kipindi chote cha nyuma. “Amesema ameridhishwa na hali ya usalama iliyopo ndani ya nchi hiyo, na akashauri wakimbizi waanze kurejea nchini mwao ili waende kuijenga nchi yao na kushiriki kwenye masuala ya maendeleo.”
Kesho (Jumapili, Septemba 22, 2024), Waziri Mkuu anatarajiwa kushiriki ufunguzi rasmi wa Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA79) ambako atajumuika na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa 193 na pia atatoa salamu za Serikali.
Kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu ni “Hakuna kuachwa nyuma yeyote: Kushirikiana pamoja kuendeleza amani, maendeleo endelevu na heshima ya binadamu kwa vizazi vya sasa na vijavyo” (Leaving no one behind: Acting together for the advancement of peace, sustainable development and human dignity for present and future generations).