Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amewasili Jijini New York nchini Marekani kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA77).

Kwa Mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango anatarajiwa kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika Ukumbi wa Mikutano wa Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini Marekani tarehe 22 Septemba 2022.

Makamu wa Rais pia akiwa Jijini humo ataongoza Ujumbe wa Tanzania katika mikutano mbalimbali ya ngazi za juu na ya pembezoni inayohusu Uchumi, Elimu, Afya, Demokrasia na Malengo ya Maendeleo Endelevu ambayo imeandaliwa na Umoja wa Mataifa.

Mkutano huo wa UNGA wa 77 unatarajiwa kujadili masuala mbalimbali ya kimataifa ambayo yameikumba dunia kwa wakati huu kama vile mlipuko wa ugonjwa wa COVID 19, Vita ya Urusi na Ukraine, mabadiliko ya tabia nchi na athari zake katika uchumi wa dunia.

Katika mkutano huo, Makamu wa Rais ameambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb.), Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (Mb.), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Zanzibar Mhe. Masoud Ali Mohamed na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Mohamed Mussa

  • Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (wa kwanza kulia) na Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa Mhe. Prof. Kennedy Gaston (katikati) alipowasili katika Ofisi za Ubalozi jijini New York kwa ajili ya kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA77).
  • Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango akizungumza na ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA77) alipowasili katika Ofisi za Ubalozi jijini New York kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano huo