Wakati hali ya kisiasa na kiusalama ikiendelea kuwa ya sintofahamu Nchini Burundi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ameelezea kutiwa moyo na juhudi mbambali zinazolenga kurejesha hali ya amani na usalama nchi humo.

Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Katibu Mkuu, siku ya Ijumaa hapa Umoja wa Mataifa, imesema, katibu Mkuu anatiwa moyo na juhudi zinazofanywa na makundi mbalimbali ya kikanda, ya kidini, ya kijamii, vyama vya siasa pamoja na Mwakilishi Wake Maalum katika Eneo la Maziwa Makuu katika kuhakikisha kwamba mgogoro na sitofahamu iliyoikumba Burundi inatafutiwa ufumbuzi.

Wahusika wakuu ambao Ban Ki Moon ameelezea kutiwa moyo na juhudi zao za kuleta amani nchini Burundi ni pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambayo ipo chini ya uenyekiti wa Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Umoja wa Afrika ( AU), Soko la pamoja la Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika ( COMESA), Mkutano wa Kimataifa wa Eneo la Maziwa Makuu ( ICGLR) na Mwakilishi wake Maalum katika eneo la maziwa Makuu Bw. Said Djinnit.

“Katibu Mkuu anawapongea washirika wote wanaoshiriki mchakato huo pamoja na mafanikio yaliyofikiwa hadi sasa, hususani katika kupunguza hali ya wasiwasi na sintofahamu na kujenga mazingira ya kufanyika kwa uchaguzi huru, wa haki, jumuishi na wa amani.” Inasomeka Taarifa ya katibu Mkuu.

Hata hiyo pamoja na kutiwa moyo na kazi nzuri inayoendelea kufanyika, Katibu Mkuu ameelezea wasi wasi wake hali mbaya ya kibinadamu inayowakabiri wakimbizi kutoka Burundi ambao wamekimbilia nchi za jirani ikiwamo Tanzania.

Pamoja na wasiwasi huo Ban Ki Moon amezipongeza nchi jirani kwa kutoa misaada ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwahifadhi wakimbizi hao. Huku akitoa wito kwa Serikali ya Burundi kuandaa mazingira ya kuwarejesha nchi humo raia wake waliokimbia machafuko.

Vile vile Katibu Mkuuu, amewahimiza wadau mbalimbali kuendelea na majadiliano kwa lengo la kufikia makubaliano ya jumla katika maeneo yote ambayo wameyaainisha. Huku akithibitisha utayari wa Umoja wa Mataifa katika kuwasaidia wananchi wa Burundi na Kanda kwa ujumla katika mchakato huu.

Taarifa kutoka Mashirika ya Kimataifa likiwamo la wakimbizi, UNHCR zinazonyesha kwamba tangu mwezi Aprili mwaka huu, jumla ya wananchi 100,000 wa Burundi wakimbia nchi yao na kuvuka mipaka na kuingia katika nchi za Tanzania, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Wimbi hilo la wakimbizi, limesababisha kuibuka kwa ugonjwa wa kipindupindu katika kambi iliyoko Kigoma ugonjwa ambao umesabisha vifo vya watu 37 kwa mujibu wa UNHCR na kwamba Serikali ya Tanzania imekwish kutangaza uwepo wa ugonjwa huo.

- Na Mwandishi Maalum, New York