Mkutano wa 69 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, uliokuwa chini ya urais wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda Bw, Sam Kutesa umefikia ukingoni siku ya jumatatu kwa kupitisha maamuzi ya kihistoria ambayo pamoja na mambo mengine yanatoa mwelekeo wa majadiliano kuhusu marekebisho na mageuzi ya Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Maamuzi hayo ambayo kwa mara ya kwanza yanaingizwa rasmi katika nyaraka muhimu za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na yaliyopewa namba A/69/L.92 yalipitishwa kwa kauli moja na wajumbe kutoka nchi 193 wanaounda Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Maamuzi hayo ambayo baadhi ya wazungumzaji waliyapachika jina kama maamuzi ya Kutessa ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake katika kusimamia kidete majadiliano kuhusu mageuzi ya Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa yanatoa msingi au maandishi ambayo kwayo yatawawezesha nchi wanachama kujadiliana kwa kupitia maamuzi hayo.
Ingawa maamuzi hayo yamepita bila la kupigiwa kura na kupongezwa kwa kufungua ukursa mpya katika kuendeleza mchakato wa majadiliano ya mageuzi na upanuzi wa Baraza Kuu la Usalama, baadhi ya nchi zimeyaelezea maamuzi hayo kuwa na ni ya kiufunzi zaidi na hivyo yasikuchukuliwe kama maamuzi ya mwisho kwa madai kwamba maandalizi na majadiliano ya maamuzi hiyo hayakuwa jumuishi na hivyo hayawakilishi maoni na hisia za makundi yote.
Akiungana na wazungumzaji wengi waliounga mkono kupitishwa kwa maamuzi hayo Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manoni, amesema , majadiliano yaliyopelekea kupatikana kwa maamuzi hayo hayakuwa rahisi, lakini yameasisi hatua mpya ya mwendelezo wa ajenda ya kulifanyia mageuzi Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa ili liwe jumuishi kuendana mazingira ya sasa.
Akasema hapana shaka kwamba majadiliano Zaidi yanapashwa kuendelea ili kijibu kiu ya kila upande na kwamba nchi wanachama wanapashwa kujivunia hatua hiyo muhimu hataka kama ni hatua ndogo.
Akatumia fursa hiyo kuwapongeza Bw.Sam Kutesa na Mwakilishi wa kudumu wa Jamaica Balozi Rattray kwa kazi nzuri kubwa na iliyokuwa na changamoto nyingi lakini iliyofanikisha kupatika kwa maamuzi hiyo.
Majadiliano kuhusu namna ya kuboresha na kupanua wigo wa wajumbe wa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, ni majadiliano yaliyoanza mwaka 2008 lakini ni katika Mkutano wa 69 wa Baraza Kuu la Umoja wa Maifa ambapo matokeo ya majadiliano miongoni mwa wanachama yameweza kupitishwa rasmi katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Muundo wa sasa wa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo linawajumbe wa kudumu na wenye kura ya turufu watano na wajumbe 10 wanaoingia kwa mzunguko wa uwakilishi wa kikanda haujaitendea haki Afrika bara ambalo licha ya kwamba asilimia kubwa ya maamuzi yanayofanywa na Baraza Kuu la Usalama yanaihusu Afrika lakini Afrika si mwanachama wa kudumu na hiyvo imekuwa ikipigania kupata nafasi ya uwakilishi wa kudumu pamoja na kura ya turufu.
Kumalizika kwa Mkutano wa 69 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kunafungua kuanza kwa Mkutano wa Baraza Kuu la 70 ambalo kwa mwaka mzima litakuwa chini ya Urais wa Bw.Monges Lykketoft.
