Mtandao wa Kijamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania ( MJUMITA) ni kati ya Asasi 21 ambazo jana ( jumatatu) zimetangawa kuwa washindi wa Tuzo ya Ikweta (Equator Prize ) kwa mwaka 2015.
Tuzo hiyo ya Ikwete hutolewa na Mfuko wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa ( UNDP) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaofadhili tuzo hiyo. Kila NGO iliyoshinda Tuzo hiyo inanyakua kitita cha dola 10,000 za Kimarekani.
Ushindi wa MJUMITA pamoja na NGO nyingine 20 ulitangazwa na Mkuu wa UNDP Bi. Helen Clark katika mkutano wake na wawakilishi wa Muungano wa Waandishi wa Habari wa Umoja wa Mataifa.
Wawakilishi wa NGO hizo 21 watapokea Tuzo zao mwezi Desemba wakati wa Mkutano wa Kimataifa utakaojadili mabadiliko ya Tabia nchi ( COP21) utakofanyika Paris, Ufaransa.
MJUMITA ni mtandano wenye wanachama katika vijiji 450 vilivyopo katika Wilaya 23 za Tanzania na hujishughulisha na utunzaji wa misitu, kuwasaidia wanavijiji kupata hati za kimila za kumiliki ardhi, kutatua migogoro inayohusisha masuala ya ardhi na kubuni miradi ya matumizi sahihi ya ardhi pamoja na raslimali za misitu.
Zaidi ya watu 500,000 wamenufaika na huduma zinazotolewa na MJUMITA.
Akizungumza wakati wa kuwatangaza washindi hao Bi Helen Clark, aliyefuatana na Bi. Christiana Figueres anayeshughulika masuala ya mabadiliko ya tabia nchi na Bw. Alec Baldwin ambaye ni mcheza sinema maarufu na mwanaharakati wa mazingira.
Amesema kuwa NGO hizo ambazo zinajihusisha Zaidi na utunzaji wa mazingira, kupambana na umaskini , utunzaji wa ardhi na matumizi endelevu ya ardhi na misitu wamedhihirisha kwamba wanalo jambo la kuifundisha Jumuiya ya Kimataifa.
Akaongeza kwamba Zaidi ya washiriki 100 waliingia katika shindano hilo lakini 21 ndio walioibuka kidedea, huku akisisitiza kila NGO ilizoibuka mshindi ina hadhithi ya aina yake yenye funzo Jumuiya ya Kimataifa.
Akasema kupitia kazi nzuri zinazofanywa na asasi za kijamii pasipo kutumia gharama kubwa au teknolojia za hali ya juu imedhihirika kwamba kuna juhudi ambazo zinatoa matokeo na watu wengi hasa maskini wanasaidia na hali yao ya maisha inaboreka na maliasili ikiwamo misitu na ardhi.
Akasisitiza kwamba, juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ni juhudi mtambuka zinazopwashwa kumshirikisha na kumjumuisha kila mutual kuanzia mtu wa kawaida ambaye haswa ndiye muathirika mkuu.
Bi. Helen Clark anaongeza kuwa Tuzo hiyo inatolewa katika kipindi ambacho Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali wanakusanyika Jijini New York kwa mkutano wao maalum wa kupitisha Ajenda 17 za Maendeleo Endelevu, ambapo ajenda namba 13 inazungumzia kwa kina mabadiliko ya tabia nchi wakati ajenda namba 15 inazungumzia uhifadhi wa viumbe anuwai, Misitu na kukabiliana na jangwa.
Akasema Mkutano huu wa kupitisha ajenda za maendeleo endelevu zinazochukua nafasi ya malengo ya maendeleo ya millennia yanayomaliza muda wake mwaka huu, unatangulia mkutano mwingine muhimu na unaosubiliwa kwa shauku kubwa , mkutano wa Mbadiliko ya Tabia nchi ( COP21).
MJUMITA ni kati ya NGO Sita kutoka Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, zilizojinyakulia tuzo hiyo. NGO nyingine zilizoshinda Tuzo Nane zinatoka Asia na Pacific na NGO nyingine Nane ni kutoka Latin Amerika na Visiwa vya Karibbean.
