Akizungumza kwa masikitiko makubwa wakati wa hafla hiyo, Katibu Mkuu, Ban Ki Moon, amesema, katika maadhimisho yote yanayofanyika katika Umoja wa Mataifa, hakuna adhimisho lenye kutia simanzi na ngumu kama hili la kuwakumbuka na kuwaenzi walinda amani ambao wamepoteza maisha yao wakati wakitoa ulinzi kwa watu wengine.

“Ninasikitika kusema kwamba, hii ni mara ya saba mfululizo ambapo zaidi ya walinda amani 100 wamepoteza maisha katika kipindi cha mwaka mmoja. Hatari wanayokumbana nayo walinda amani wetu inazidi kuongezeka kwa kasi kubwa, kutoka kushambuliwa na makundi ya wahafidhina na makundi ya wanamgambo wenye silaha mpaka hatari ya magonjwa ambukizi kama vile Ebola” amesema katibu Mkuu.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa akaendelea kusema. “ Tumekusanyika hapa kuwaenzi mashujaa wetu waume kwa wake ambao wamepoteza maisha yao wakati wakiwalinda wananchi katika maeneo hatari duniani. Kujitoa kwao muhanga na namna walivyoyaishi maisha yao, wanatufanya sisi tujisikie fahari na kututia shime ya kufanya kazi kwa bidii zaidi ili kudhihirisha kwamba maisha yao hayakupotea bure.

Ban Ki Moon, awaeleza wawakilishi kutoka nchi ambazo zimepoteza mashuja wake kwamba, operesheni za ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa zitaendelea kuwa zenye changamoto na hatari kubwa, na cha kusikitisha ni kwamba adhimisho lililofanyika ijumaa la kuwaenzi mashujaa hao halitakuwa la mwisho.

“Walinda amani wetu wanabeba jukumu zito kwaajili yetu sote. Natoa heshima zangu kwa mashujaana salamu zangu za pole kwa familia za mashujaa hawa” akasisitiza Katibu Mkuu.

Walinda amani hao 126 na raia 19 wamepoteza maisha wakati wakihudumua katika misheni zilizopo, Afghanistan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Ivory Coast, Cyprus, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Haiti, Mali, Mashariki ya Kati, Liberia, Sudan na Sudan ya Kusini.

Pamoja na Tanzania nchi nyingine ambazo zimepoteza mashujaa wake katika misheni mbalimbali za kulinda Amani katika mwaka uliopita ni Senegal, Afrika ya Kusini, Uhispania, Togo, Rwanda, Benin, Burkina Faso, Bangladesh,na Burundi.

Nyingine ni Cambodia, Chad, El Salvador, Ethiopia, Fiji, France, Ghana, India, Indonesia, kenya , Malawi, Niger, Pakistan, Philippines, Tunisia na Zimbabwe.

Pamoja na mashujaa hao ambao ni wanajeshi, wapo pia raia 19 wakiwamo pia polisi, madaktari, watumishi na watoa misaada ya kibinadamu ambao wamepoteza maisha wakati wakitoa misaada kwa binadamu wenzao.

Wakati Umoja wa Mataifa ukiwaenzi mashujaa hao waliopoteza maisha mwaka jana. Tayari mwaka huu wa 2015 mashujaa wapatao 49 wamekwisha poteza maisha wakitekeleza majukumu yao ya kuleta Amani , utulivu na ulinzi wa raia wasio na hatia katika nchi zenye migogoro. Kati ya mashujaa 49 hao wapo watanzania wawili.

Jumla ya walinzi wa Amani 3,300 wamekwisha kupoteza maisha tangu kuanzishwa kwa Operesheni za Ulinzi wa Amani chini ya Umoja wa Mataifa mwaka 1948.

- Na Mwandishi Maalum, New York

  • Charge d’ affaires a.i Maura Mwingira wa Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, akiandika katika kitabu maalum, baada ya kupokea kwa niaba ya familia za mashujaa wanne wa JWTZ waliopoteza maisha wakati wakihudumu katika misheni za kulinda amani mwaka jana. Medali hiyo maalum ya Dag Hammarskjold ilitokwa siku ya ijumaa kama ishara ya kuwaenzi, kutambua na kuthamini mchango mkubwa wa mashujaa hao.
  • Katibu Mkuu Ban Ki Moon, akiwa na Naibu Katibu Mkuu, Jan Eliasson, na Viongozi wakuu wa Idara ya Operesheni za Ulinzi wa Amani ( DPKO) muda mfupi kabla ya utoaji wa medali maalum kwa mashujaa 126 walinda amani ambao walipoteza maisha mwaka jana. katika salamu zake Katibu Mkuu alieleza kwamba katika maadhimisho yote yanayofanyika katika Umoja wa Mataifa, adhimisho la kuwakumbuka na kuwaenzi walinda amani ni adhimisho lenye kutia simanzi na gumu.
  • Mpiga Buluji akiimba wimbo maalum wa maombolezo kama ishara ya kuwakumbuka mashujaa 126 walinda amani waliopoteza maisha mwaka jana. shughuli za utoaji wa medali maalum zilitanguliwa na uwekaji wa shada maalum la maua katika eneo ambalo limetengwa katika viunga vya Umoja wa Mataifa . Pichani anaonekana Katibu Mkuu Ban Ki Moon akitoa salamu za heshima kwa wahanga hao anaonekana pia Naibu Katibu Mkuu Jan Eliasson.