Jumuiya ya Kimataifa imemuelezea aliyekuwa Katibu Mkuu wa Sita wa Umoja wa Mataifa, Marehemu Boutros Boutros- Ghali, kama kiongozi ambaye siyo tu alifanya kazi katika mazingira magumu lakini pia alitoa mchango mkubwa katika kuijenga na kuimarisha Taasisi hiyo ya Kimataifa.

“Leo tumekusanyika hapa kutambua na kuheshimu mchango mkubwa wa mtangulizi wangu katika kukijenga na kukiimarisha chombo hiki. Hapana shaka aliingia katika kipindi kigumu mwishoni mwa vita baridi” akaeleza Ban Ki Moon.

Jana ( alhamisi) Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa likiongozwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa litenga muda maalum wa kumuenzi na kukumbuka mchango mkubwa wa Marehemu Boutros Boutros Ghali.

Katibu Mkuu Ban Ki Moon, katika salamu zake amebainisha kwamba, pamoja na mazingira magumu ya utekelezaji wa majukumu yake, na hasa ikizingatiwa kwamba alishika wadhifa huo mwisho wa vita baridi,bado aliweza kuweka misingi mingi mizuri ikiwamo ya uboreshaji wa Operesheni za Ulinzi wa Amani kupitia kofia ya Umoja wa Mataifa pamoja na utendaji wa sekretarieti ya Umoja wa Mataifa.

“Alikuwa mpenda Amani, usalama, haki za binadamu, mwanadiplomasia, msomi na mwanazuoni aliyebobea ambaye hakuogopa kusema ukweli na kusimamia kile alichokiamini”. Akasema Ban Ki Moon.

Marehenu Boutros Boutros- Ghali ambaye amefariki siku ya jumanne akiwa na miaka 93 alikuwa Katibu Mkuu wa Kwanza kutoka Barani Afrika na Mwarabu wa Kwanza.

Wazungumzaji wengi waliozungumza kwa niaba ya Kanda zao wanazoziwakilisha walieleza kwamba Jumuiya ya Kimataifa ilikuwa imeondokewa na mtu mashuhuri ambaye bado alikuwa na mchango mkubwa katika diplomasia ya kimataifa.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kudumu wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Balozi Samantha Power, katika salamu za serikali yake, amemuelezea Boutros Boutros- Ghali kama kiongozi ambaye alikuwa na uzoefu mkubwa katika uendeshaji wa majadiliano .

Akataja baadhi ya mafanikio yaliyotoka na usimamizi na uongozi wake ni pamoja na kuushawishi utawala wa Makaburu wa Afrika ya Kusini kumwachia huru Marehemu Mzee Nelson Mandela.

Pamoja na kueleza kwamba Boutrous Boutrous – Ghali alikuwa kiongozi mwenye vipaji vipingi, na aliyefanya mengi katika diplomasia ya Umoja wa Mataifa, lakini pia akaeleza wazi kwamba serikali yake ( Marekani) mara kwa mara ilitofautiana na Katibu Mkuu Boutros Ghali.

Na akaongeza kwamba pamoja na kutofautiana huko bado Marekani inaheshimu na kutambua mchango mkubwa wa Katibu Mkuu huyo wa Sita. Na kusisitiza kwamba Jumuiya ya Kimataifa inapashwa kuyaendeleza na kuyadumisha mema ya Marehemu Boutros Ghali.