Tanzania kuendelea kuiunga mkono Mahakama ya Afrika ya Haki za binadamu na watu katika kuhakikisha utoaji haki kwa wananchi unatekelezeka kwa wakati, uwazi na uadilifu.

Makamu wa Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amebainisha hayo wakati wa kufungua Mdahalo wa tano wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu jijini Dar es Salaam.

Amesema Tanzania itaendelea kuiunga mkono Mahakama hiyo katika kuhakikisha inatekeleza majukumu yake na kuongeza kuwa itaendelea kuwa mwanachama wa Mahakama hiyo kutokana na ukweli kuwa ni miongoni mwa nchi zilizoshiriki kikamilifu katika kuanzishwa kwa mahakama hiyo.

Ameongeza kuwa lengo la kuanzishwa kwa Mahakama hiyo ilikuwa ni pamoja na kuzisaidia Mahakama za nchi wanachama katika utoaji haki kwa kutekeleza maamuzi ya Mahakama hiyo na siyo kukinzana na Mahakama na sheria za nchi wanachama  kupitia utekelezaji wa maamuzi yake.

‘Tanzania itaendelea kuwa mwanachama, tulishiriki katika uanzishwaji wake, tutaendelea kuwa sehemu ya Mahakama hii kwa kuzingatia kuwa Mahakama hii ilianzishwa kwa lengo la kuzisaidia mahakama za nchi wanachama na sio kukinzana na mahakama na sheria za nchi wanachama,’ amesema Dkt. Mpango.

 Amewataka washiriki wa mdahalo huo kupitia majadiliano yao kuja na mapendekezo yatakayosaidia na kuwezeha upatikanaji wa haki kwa wananchi wote kwa wakati badala ya kukinzana na sheria za nchi wanachama.

Amesema utoaji haki kwa wananchi wote ndio jambo la msingi na kwamba mfumo wa utoaji haki  hauna budi kuimarishwa ili kutekeleza jukumu hilo kwa nguvu zote kwani imani ya wananchi kwa mfumo huo ndio msingi wa imani ya wananchi .

Awali akizungumza katika ufunguzi wa Mdahalo huo, Rais wa Mahakama hiyo Mhe. Jaji Imani Aboud amesema mdahalo wa mwaka huu umejikita katika kuangalia ufanisi na utekelezaji wa majukumu ya mahakama.  

Naye mwakilishi wa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Jaji Dkt. Deo John Nangela kutoka Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara amesema Tanzania ina mahusiano makubwa na taasisi za Kimataifa ikiwemo Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na Mahakama nyingine zilizoko katika kanda na kuongeza kuwa Tanzania ni mdau katika mahakama hizo na itaendelea kuziunga mkono mahakama hizo katika kuhakikisha utoaji haki unapatikana kwa wakati na uwazi.

Mdahalo wa Tano wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na watu unahudhuriwa na majaji na Wanasheria wa Serikali kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika na kauli mbiu yake inasema kujenga imani kwa mfumo wa mahakama wa Afrika.